Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wingi wa sampuli za kupima Kipindupindu Kigoma, ulinifanya nivae magwanda niingie kazini: Lusekelo

Wingi wa sampuli za kupima Kipindupindu Kigoma, ulinifanya nivae magwanda niingie kazini: Lusekelo

Mwishoni mwa mwezi uliopita wa Mei, mlipuko wa ugonjwa wa Kipindupindu uliripotiwa huko Kigoma nchini Tanzania kufuatia wimbi la wakimbizi wa Burundi waliokuwa wanakimbilia nchi jirani kusaka hifadhi baada ya mzozo kuibuka nchini mwao. Uhaba wa huduma za kutosha za majisafi na kujisafi uliibua changamoto na mlipuko kuripotiwa miongoni mwa wakimbizi hasa kwenye kijiji cha Kagunga kilichoko mpakani, halikadhalika kambini Nyarugusu. Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na shirika la afya duniani, WHO walihaha kutwa kucha kudhibiti mlipuko huo uliosababisha vifo vya watu 30 na wengine zaidi ya 4,400 kuambukizwa. Jitihada hizo ni pamoja na kutuma wataalamu wa afya wakiwemo wanasayansi wa maabara miongoni mwao Jacob Lusekelo, mwanasayansi wa maabara kutoka Maabara kuu ya Taifa nchini Tanzania. Akihojiwa kwa njia ya simu kutoka Tanzania na Assumpta Massoi wa Idhaa hii,  Bwana Lusekelo anaelezea kile walichofanya na jinsi huduma yao ilivyosaidia kudhibiti mlipuko. Kwanza anaelezea hali ilivyokuwa walivyowasili Kigoma.