Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kipindupindu miongoni mwa wakimbizi wa Burundi chaanza kudhibitiwa:WHO-Tanzania

Kipindupindu miongoni mwa wakimbizi wa Burundi chaanza kudhibitiwa:WHO-Tanzania

Shirika la afya duniani, WHO nchini Tanzania limesema idadi ya maambukizi mapya ya ugonjwa wa Kipindupindu miongoni mwa wakimbizi wa Burundi waliokimbilia mkoani Kigoma nchini Tanzania imepungua baada ya visa zaidi ya 4,400 kuripotiwa na wagonjwa 30 kufariki dunia huku kisa kimoja cha awali kikibainika kuwa hakikuwa Kipindupindu. Amina Hassan na maelezo zaidi.

(Taarifa ya Amina)

WHO imesema visa vipya vya kipindupindu kwa siku vimepungua kutoka 915 tarehe 18 mwezi huu hadi 100 kwa sasa na hali hiyo imesababishwa na hatua zilizochukuliwa kudhibiti mlipuko ikiwemo kuimarisha huduma za kujisafi.

WHO inasema harakati za kudhibiti Kipindupindu zinafanywa kwa ushirikiano baina ya serikali ya Tanzania na wadau kama vile Umoja wa Mataifa na madaktari wasio na mipaka, MSF.

Dokta Rufaro Chatora ni mwakilishi wa WHO nchini Tanzania.

(Sauti ya Dkt. Rufaro)

"Licha ya  visa vya kipindupindu kushuka katika siku chache zilizopita, hali bado ni mbaya mno, mbali na kipindupindu sisi pia tunasimamia shughuli zingine za kiafya mathalani kwa siku kuna wazazi 72 wanajifungua na kati yao  17 ni Kagunga."

Wakati huo huo shirika la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR limesema idadi ya wakimbizi wa Burundi wanaoingia Tanzania imepungua kama anavyoeleza msemaji wake Adrian Edwards.

(Sauti ya Adrian)

"Kazi inafanywa ili kupanua uwezo wa kambi katika ukanda mzima, mmiminiko wa wakimbizi kutoka Burundi haujapungua lakini kiwango sasa kimepungua na tunapata wakimbizi 100 kwa siku katika nchi zinazopokea wakimbizi, tukizingatia takwimu mpya tumepokea zaidi ya wakimbizi 90,000 katika ukanda huu, ikiwa ni pamoja na 10,000 DRC, 47,000 Tanzania na 28,000 Rwanda na 5,500 Uganda. "

Umoja wa Mataifa unasema kijiji cha Kagunga ambacho ndio kilikuwa kitovu cha mlipuko sasa wakimbizi wote wanakaribiwa kuondolewa ili kazi ya kupulizia dawa kukinga maambukizi mapya iweze kufanyika.