Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hakuna tena visa vya Ebola Liberia: WHO

Hakuna tena visa vya Ebola Liberia: WHO

Shrika la afya ulimwenguni WHO leo limetangaza kuwa Liberia moja ya nchi iliyokumbwa na mlipuko wa homa kali ya Ebola, haina tena visa hivyo baada ya siku 42 kupita pasina kisa chochote.

Kwa mujibu wa WHO kisa cha mwisho cha Ebola kilikuwa March 28 mwaka huu, na hivyo kupongeza taifa hilo la Afrika Magharibi.Shirika hilo la afya ulimwenguni limesema wakati wa mlipuko huo mkubwa zaidi tangu Ebola ilipogundulika mwaka mwaka 1976, Liberia iliripoti visa vipya 300 hadi 400 kwa wiki.

Mlipuko huo ulisababisha athari za kiuchumi na kijamii kwa taifa hilo na ukanda mzima wa Magharibi mwa Afrika.

Licha ya pongezi kwa serikali na wadau wa afya kwa kupambana na Ebola, WHO imeitahadharisha serikali ya Liberia kuwa makini zaidi ili gonjwa hilo lisirejee tena na kusema kuwa taifa hilo lina uzoefu na uwezo pamoja na usaidizi kutoka jumuiya ya kimataifa.

Shirika la afya ulimwenguni WHO hata hivyo limesema katika taarifa yake kuwa wafanyakazi wake watasalia nchini humo hadi mwisho wa mwaka ili kuhakikisha hali ya afya inarejea kuwa ya kawaida.