Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukwepaji sheria kwa wanaoshambulia walinda amani ukome:UNAMID

Ukwepaji sheria kwa wanaoshambulia walinda amani ukome:UNAMID

Kaimu Mkuu wa ujumbe wa pamoja wa Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika huko Darfur nchini Sudan, UNAMID Abiodun Bashua amelaani mashambulizi mawili yaliyofanyika jana na leo huko Darfur Kusini, ambayo hata hivyo walinda amani wake wameweza kuyajibu na kuokoa baadhi ya mali zilizokuwa zimeibwa.

Kwa mujibu wa taarifa ya UNAMID,  Ijumaa asubuhi walinda amani hao wakiwa doria walijibu shambulio dhidi yao huko Kass kilometa 83 Kaskazini-Magharibi mwa Nyala Darfur Kusini ambapo washambuliaji wapatao wanne waliuawa huku walinda amani sita wakijeruhiwa.

Halikadhalika Alhamisi jioni watu wapatao 40 wenye silaha wakiwa kwenye farasi na ngamia walishambulia walinda amani wa Nigeria waliokuwa doria kwenye kituo cha maji na kuiba gari la ujumbe huo baada ya kumshambulia dereva.

Hata hivyo walinda amani hao waliweza kuwafuatilia na kuokoa gari hilo.

UNAMID inasema walinda amani waliojeruhiwa wanapatiwa tiba huko Nyala huku Kaimu Mkuu huyo wa UNAMID akiwatakia ahueni ya haraka.

Bwana Bashua ametoa wito kwa serikali ya Sudan kuchunguza tukio hilo na kuwafikisha mbele ya sheria wahusika wa tukio hilo akisisitiza umuhimu wa kukomesha tabia ya ukwepaji wa sheria kwa watu wanaoshambulia walinda amani na watoa  huduma za kibinadamu.