Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban awa na mazungumzo Waziri Mkuu wa Lebanon nchini Kuwait

Ban awa na mazungumzo Waziri Mkuu wa Lebanon nchini Kuwait

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon aliyeko ziarani Mashariki ya Kati amekuwa na mazungumzo na Waziri Mkuu wa Lebanon, Tammam Salam kando mwa mkutano wa wahisani wa Syria nchini Kuwait.

Katika mazungumzo yao, Ban amemshukuru kwa nchi yake kujitoa kwa hali na mali kusaidia wakimbizi wa Syria huku akielezea azma ya Umoja wa Mataifa ya kupunguza makali wanayopata nchi zinazohifadhi wakimbi hao.

Amesema Umoja wa Mataifa unaendelea kusihi jamii ya kimataifa kuendelea kusaidia Lebanon.

Ban ametumia fursa hiyo pia kumpongeza Waziri Mkuu Salam kwa uongozi wake katika kuzingatia umoja wa kitaifa akisema ni matumaini yake kuwa vyama vya siasa nchini Lebanon vitamaliza tofauti zao na kupatia suluhu masuala yaliyosalia ikiwemo uchaguzi wa Rais.

Halikadhalika Ban amemshukuru Waziri Mkuu huyo kwa ushiriki wake katika kusaidia majukumu ya mratibu maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Lebanon pamoja na Mkuu wa ujumbe wa ulinzi wa amani wa umoja huo Kusini mwa Lebanon Meja Jenerali Luciano Portolano.