Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF yataka watoto walindwe Yemen

UNICEF yataka watoto walindwe Yemen

Takribani watoto 62 wameuawa na wengine 30 wamejeruhiwa katika wiki moja iliyopita ya mapigano nchini Yemen.

Takwimu hizo ni kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF, likisema mapigano hayo pia yamesambaratisha huduma za msingi za afya, elimu huku watoto wakisalia na kiwewe.

Mwakilishi wa UNICEF nchini Yemen Julien Harneis amesema watoto wanahitaji ulinzi wa hali ya juu na hivyo pande husika kwenye mzozo huo lazima zihakikishe watoto wako salama.

Amesema hali ya kibinadamu inavyozidi kuzorota nchini Yemen,  inatowesha zaidi hali ya watoto ambayo tayari ilikuwa imedorora, sanjari na ukosefu wa usalama wa chakula, utapiamlo uliokithiri na utumikishaji watoto jeshini.

Hata hivyo amesema UNICEF na wadau wa kitaifa na kimataifa nchini humo wanaendelea kusambaza huduma muhimu kama vile maji, huduma za kujisafi, chanjo na lishe pamoja na mipango ya kusaidia watoto waliokumbwa na kiwewe kutokana nay ale wanayoshuhudia.