Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkutano wa usaidizi Syria wafanyika leo Kuwait

Mkutano wa usaidizi Syria wafanyika leo Kuwait

Nchini Kuwait hii leo kunafanyika mkutano wa Tatu wa kimataifa kuhusu usaidizi wa Syria ambapo Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu misaada ya kibinadamu Valerie Amos amesema mzozo huo unazidi kuzorotesha hali ya kibinadamu.

Akihojiwa na Radio ya Umoja wa Mataifa, Bi. Amos amesema licha ya wahisani kujitoa kwa hali na mali, mathalani mwaka jana ambapo walipata asilimia 90 ya ahadi za kwenye mkutano wa pili wa usaidizi, bado mahitaji yanaongezeka.

Amesema mahitaji ya kibinadamu yanaongezeka siyo tu Syria, lakini pia maeneo mengine akitolea mfano Yemen hivyo amesema..

(Sauti ya Amos)

“Sote tunafahamu kuwa suluhu la kisiasa ni lazima lipatikane, yaani ghasia tunazoshuhudia kila siku ni lazima zikome. Hii italeta mabadiliko makubwa ndani ya Syria.”

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ndiye atakuwa mwenyekiti wa mkutano huo utaokuwa chini ya uenyeji wa kiongozi mkuu wa Kuwait Sheikh Sabah Al-Ahmad Al-Jaber Al-Sabah.

Bi.Amos ambaye pia ni mkuu wa ofisi ya usaidizi wa kibinadamu ya Umoja wa Mataifa, OCHA amemshukuru wahisani kwa kuendelea na moyo wa kujitoa kwa hali na mali, halikadhalika Kuwait kwa kusimamia mkutano huo.

Wakati mzozo wa Syria umeingia mwaka wa Tano, Umoja wa Mataifa unasema watu zaidi ya Milioni 12 wamesalia katika mahitaji makubwa ya usaidizi.