Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Biashara mtandao ni fursa lakini umakini wahitajika: UNCTAD

Biashara mtandao ni fursa lakini umakini wahitajika: UNCTAD

Ripoti mpya ya kamati ya biashara na maendeleo ya Umoja wa Mataifa, UNCTAD imesema kuna fursa kwa nchi zinazoendelea kunufaika na biashara mtandao, E-Commerce.

Pamoja na fursa, ripoti hiyo iliyotolewa Jumanne pia inataja hatari zitokanazo na ununuzi na uuzaji wa bidhaa kupitia mitandao.

Nchi za Afrika zilizo Kusini mwa jangwa la Sahara ni mojawapo ya maeneo ambako biashara mtandao inatabiriwa kupanuka.

Torbjörn Fredriksson, ni afisa kutoka UNCTAD kitengo cha teknolojia na vifaa.

(Sauti ya Fredriksson)

“Mosi ni kuimarika kwa uunganishaji wa intaneti, simu za mkononi na ongezeko la matumizi ya intaneti na mitandao ya kijamii. Pili kupungua kwa vikwazo kwa kampuni zinazotaka kuanzisha kufungua biashara mtandao kutokana na huduma mpya mfano zile za malipo kwa mtandao, ikilinganishwa na miaka mitatu au mitano iliyopita. Na tatu tunashuhudia ongezeko la kampuni kutoka nchi zinazoendelea ambazo zimeanza kutoa majibu ya matatizo kulingana na mahitaji ya nchi hizo mathalani kwenye biashara mtandao.”

Yakadiriwa kuwa mwaka 2013 thamani ya biashara mtandao ilikuwa zaidi ya dola Trilioni 16 huku Marekani, Uingereza, Japan na China zikiongoza katika sekta hiyo.

UNCTAD inasema biashara mtandao ni muhimu zaidi hivi sasa kuliko wakati wowote.

(Sauti ya Fredriksson)

“Huduma nyingi za kiuchumi zinauzwa kupitia mtandao na wakati mwingine zinawasilishwa kwa mtandao mfano bidhaa na huduma za kidigitali. Pia tunashuhudia usambazaji wa bidhaa uwe kitaifa na kimataifa unazidi kujihusisha na ununuzi kupitia mtandao.”

Hata hivyo UNCTAD inaonya kuwepo kwa changamoto ikiwemo uhalifu kwenye mitandao wakati wa biashara hiyo ambapo China, Brazili, Nigeria na  Vietnam zinatawa kukumbwa zaidi na uhalifu huo.