Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mapigano kusini mwa Ufilipino yakimbiza maelfu:UNHCR

Mapigano kusini mwa Ufilipino yakimbiza maelfu:UNHCR

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR limesema mapigano kusini mwa Ufilipino kati ya majeshi ya serikali na watu wanaotaka kujitenga yamesababisha watu wapatao 120,000 kukimbia makazi yao.

UNHCR inasema mapigano hayo ya wiki nane sasa kwenye manispaa 13 za eneo la Maguindanao, yamesababisha watu kusaka hifadhi kwenye majengo ya umma pamoja na shule huku wengine wakisaka hifadhi kwa ndugu na marafiki.

Shirika hilo linasema ni vigumu kufikia maeneo hayo lakini linajitahidi kuwafikia wakimbizi hao wa ndani kwa usaidizi wa mamlaka za eneo husika.

Babar Baloch ni msemaji wa UNHCR.

"UNHCR ina wasiwasi zaidi juu ya usalama wa raia hususan wanawake na watoto ambao wamenaswa kawenye maeneo yenye mapigano. Hadi sasa haifahamiki kwa muda gani mzozo huo utaendelea.”

Shirika hilo limewapatia mahitaji ya msingi wakimbizi hao wa ndani ikiwemo blanketi na vyandarua huku misaada zaidi ikihitajika kama vile vyakula, dawa, maji na makazi.

Mapigano ya sasa kati ya vikosi vya seriakli na wapiganaji wa Bangsamoro yaliibuka mwezi Januari na yameendelea licha ya makubaliano ya amani yaliyotiwa saini mwaka jana kumaliza miongo ya mapigano.