Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ebola : mgonjwa mmoja kati ya watano ni mtoto

Ebola : mgonjwa mmoja kati ya watano ni mtoto

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF, limeonya kwamba ni muhimu kutopunguza jitihada katika kupambana na mlipuko wa Ebola, kwa sababu bado ugonjwa huo haujadhibitiwa.

Katika ripoti iliyotolewa leo, UNICEF imeonyesha kwamba asilimia 20 ya visa vya Ebola ni watoto, na kwa ujumla, watoto 16,000 wamepoteza mzazi mmoja au wawili kutokana na Ebola.

Akizungumza na Redio ya Umoja wa Mataifa, Msemaji wa UNICEF, Christophe Boulierac, amesema lengo ni kutokomeza Ebola huku akieleza jinsi watoto yatima wanasaidiwa na UNICEF.

« UNICEF imefanya kazi sana na jamii, hasa familia za ukoo au familia zingine ili kuwasaidia kupokea hawa watoto na kuwalea kwenye mazingira mazuri. Kwa hiyo ni idadi ndogo ya hawa watoto 16,000 ambao wamepokelewa kwenye vituo maalum. Kipaumbele ni kuwarudishia kwenye familia, na bahati nzuri bado inawezekana kwenye ukanda wa Afrika Magharibi hasa kwenye hizo nchi tatu »

Aidha katika jitihada zake UNICEF imeripoti kupeleka maelfu ya chanjo za watoto dhidi ya magonjwa mengine kama surua, na kuzisaidia serikali katika maandalizi ya kurejesha shuleni watoto milioni tano, kwa kupunguza hatari za kuambukiza.

Hatimaye, ripoti ya UNICEF imesisitiza umuhimu wa kuwekeza katika mifumo ya afya ili kuiimarisha, na kupambana na magonjwa mengine yanayokumba watoto wa Afrika magharibi kama surua, kuhara au numonia.