Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

OCHA yajiapanga kukabiliana na madhara ya kimbunga PAM

OCHA yajiapanga kukabiliana na madhara ya kimbunga PAM

Timu ya misaada ya kibinadamu katika ukanda wa Pacific kutoka ofisi ya Umoja wa Mataifa ya misaada ya kibinadamu OCHA inahaha kuepusha athari mbaya za kimbunga huko Vanuatu.

Katika siku mbili kimbunga hicho PAM kimeathiri mataifa mengi ya visiwani yaliyoko kusini mwa bahari ya Pacific ambapo OCHA inasema kuwa kimbunga hicho kibaya na kilichoko katika daraja la 5 kitaalamu,  kilivuma kuanzia mjini Vanuatu na  Port Vila jioni ya March 13

Kwa mujibu wa OCHA janga kubwa kama hili halijashuhudiwa katika historia ya Vanuatu ambapo upepo unaokadiriwa kuwa na mwendo kasi wa kilometa 250 kwa saa ulivuma  na kusababisha uharibifu mkubwa ukiwamo wa miundombinu kama vile umeme na kuacha uchafu ukiwa umesambaa mjini.

Kimbunga hiki kinakuja wakati huu ambapo wakuu wa  nchi 186 kote duniani wako mjini Sendai Japan katika kongamano la tatu la kupunguza majanga . Mikakati thabiti itayaoibuliwa na mkutano huo huenda ikawa muarubaini katika kutatua majanga kama haya.

Akiongea katika mkutano huo Rais wa Vanuatu Baldwin Lonsdale amekaririwa akisema kuwa matumaini ya nchi yake kuelekea katika mustakabli wa mafanikio yamefififa.

 "Naongea nanyi leo nikiwa na moyo mzito sana. Sijui madhara gani kimbunga PAM kimesababisha huko Vanuatu kwa kuwa hakuna ripoti zilizothibitishwa bado."

 Mkuu wa OCHA katika ukanda wa PACIFIC Sune Gudnitz amesema timu ya misaada ya kibinadamu katika ukanda huo iko tayari kusaidia serikali kukabiliana na madhara ya kimbunga hicho.