Wajumbe wa baraza la usalama wakutana na Rais wa mpito wa CAR.

11 Machi 2015

Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wanaendelea na ziara yao huko Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR ambapo leo wanakuwa na mazungumzo na viongozi wa mamlaka ya mpito akiwemo Rais Catherine Samba-Panza kwenye mji  mkuu Bangui.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amewaambia waandishi wa habari mjini New York kuwa ziara hiyo ni ya kwanza kufanywa na baraza hilo tangu MINUSCA ianze kazi yake nchini CAR mwaka jana.

Wajumbe pia watakuwa na mazungumzo na wawakilishi wa vyama vya kiraia, wanadiplomasia na uongozi wa MINUSCA.

(Sauti ya Dujarric)

“Wajumbe wako nchini humo kutathmini harakati zilizochukuliwa katika kuleta utulivu nchini humo kwenye mwezi wa kwanza wa operesheni za MINUSCA.”

Ziara hiyo ya wajumbe wa baraza la usalama itawapeleka makao makuu ya Muungano wa Afrika, AU huko Addis Ababa, halikadhalika Burundi.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter