Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ili tukabiliane na ugaidi, lazima tutambue mizizi yake- Ban

Ili tukabiliane na ugaidi, lazima tutambue mizizi yake- Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amesema leo kuwa kukabiliana na changamoto ya ugaidi kwa njia inayolitatua tatizo badala ya kuliongeza maradufu huenda ukawa ndio mtihani mkubwa zaidi kwa familia ya ubinadamu katika karne ya 21. Taarifa kamili na Joshua Mmali

(Taarifa ya Joshua)

Katibu Mkuu ameyasema hayo leo mjini Washington D.C, Marekani, ambako unafanyika mkutano wa viongozi kutoka zaidi ya nchi 60, ukilenga kutafutia mwarobaine tatizo la ugaidi.

Ban amesema hakuna shaka yoyote kwamba kuibuka kwa makundi ya kigaidi yanayovuka mipaka ya nchi, yakiwemo Da’esh na Boko Haram, ni tishio kubwa kwa amani na usalama wa kimataifa.

“Makundi haya yanatumia mbinu inayokusudia kuleta mshtuko na kuonyesha uovu uliokithiri- kama vile kuchinja, kuteketeza na filamu zinazolenga kuzua chuki na kutia hofu- ili kutuchochea na kutugawanya. Wahanga ni watu tofauti kama ulivyo ubinadamu wenyewe. Lakini tutambue kuwa kwa wingi zaidi, wahanga ni Waislamu, ambao wanashuhudia mageuzi na dhiki”

Ban amesema ni vigumu kupambana na ugaidi bila kutambua vyanzo vyake

“Kwanza, kuzuia ukatili wenye msimamo mkali kunahitaji kutafuta mizizi yake. Kutafuta kichochezi cha misimamo mikali ni zoezi gumu mno. Lakini tunajua kuwa dhana zenye sumu hazitoki hewani. Unyanyasaji, ufisadi na ukiukaji haki ndivyo vinavyozalisha chuki.”

Katibu Mkuu amesema viongozi wenye msimamo mkali wenyewe ni wahalifu, magenge na majambazi ambao hawapo hata karibu na imani wanazodai kuwakilisha, lakini wanawanyanyasa vijana wasio na ajira au waliotelekezwa na jamii zao.