Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uwekezaji watakiwa magonjwa yasiyopewa kipaumbele:WHO

Uwekezaji watakiwa magonjwa yasiyopewa kipaumbele:WHO

Ripoti mpya ya Shirika la afya duniani, WHO imetaka nchi zilizoathirika zaidi na magonjwa 17 yaliyokuwa hayapatiwi kipaumbele, NTDs kuongeza uwekezaji ili kuokoa maisha ya watu zaidi y a Bilioni Moja duniani kote. Taarifa zaidi na Assumpta Massoi.

(Taarifa ya Assumpta)

Katika ripoti hiyo iitwayo Uwekezaji kupunguza madhara ya NTDs, WHO inataja magonjwa hayo ambayo hukumba zaidi nchi za kitropiki kuwa ni pamoja na matende,ngirimaji, malale, minyoo ya tumbo,kichocho na usubi ambayo huathiri jamii hususan maskini na kuidhoofisha na hatimaye kushindwa kushiriki shughuli za kiuchumi na kijamii.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Margaret Chan amesema kiasi cha fedha kinachotakiwa ni asilimia Sifuri Nukta Moja tu ya bajeti nzima ya afya katika nchi husika.

WHO imetolea mfano ugonjwa wa Malale ambao  uwekezaji katika kukabiliana nao umepunguza idadi ya visa vipya mwaka  2013 na kuwa chini ya 10,000 kwa mwaka,ikiwa ni mara ya kwanza ndani ya miaka 30.

Kwa mujibu wa WHO mabadiliko ya tabianchi nayo yamebadili mwelekeo wa magonjwa hayo na kuyafanya yaenee hata kwenye nchi zisizo za kitropiki.