Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Serikali ya Iraq yajitahidi dhidi ya ISIL: UM

Serikali ya Iraq yajitahidi dhidi ya ISIL: UM

Baraza la Usalama limekutana leo kujadili riopoti ya katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Iraq, wakati ambapo jitihada za kimataifa na kitaifa zinazidi ili kupambana na kundi linalotaka kuweka dola la Uislamu wenye msimamo mkali, ISIL.

Nickolay Mladenov, mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu huko Iraq na mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo, UNAMI, amelieleza Baraza la Usalama kwamba serikali ya Iraq inapaswa kupongezwa kwa jitihada zake katika kuendelea kuheshimu demokrasia na utawala wa sheria katika nyakati hizi ngumu. Aidha amekaribisha uundwaji wa serikali jumuishi septemba mwaka jana.

Hata hivyo, amesema, Iraq inakumbwa na janga la ugaidi, akieleza kwamba watu zaidi ya 12,000 wamefariki dunia mwaka jana kwa sababu ya vita:

“ ISIL inaendelea kutawala sehemu nyingi ya mikoa ya magharibi mwa nchini. Jitihada za maridhiano na umoja zinazoendelea taratibu zinapaswa kukuzwa kwa umakini ili zilete mafanikio, na kushuka kwa bei ya mafuta kumeathiri uchumi na kuongezeka kwa gharama za usalama”  

Mladenov amesikitishwa na ripoti za ukiukwaji wa haki za binadamu unaotekelezwa na ISIL, hasa dhidi ya watoto, wanawake, na mwakundi ya watu walio wachache, huku mashambulizi ya kigaidi yakitishia raia wa Iraq karibu kila siku.