Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Asilimia 61 ya wananchi wa Yemen wanahitaji msaada:OCHA

Asilimia 61 ya wananchi wa Yemen wanahitaji msaada:OCHA

Ofisi ya uratibu wa misaada ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa, OCHA, imekuwa na kikao maalum jijini New York, kuhusu hali ya kibinadamu nchini Yemen ambako kwa mujibu wa ofisi hiyo asilimia 61 ya wananchi wote wanahitaji msaada wa dharura.

Mkuu wa operesheni wa OCHA John Ging akifungua kikao hicho amesema hali ya sasa ni  ya mashaka makubwa na hata mwelekeo wa hali ya kibinadamu na usalama iko mashakani.

Akihutubia kwa njia ya video kutoka Morocco, mratibu mkuu wa OCHA nchini Yemen Johannes Van Der Klaauw amesema hakuna huduma za afya, kuna ukiukwaji mkubwa wa haki za msingi na shughuli za kiuchumi zimekwama.

(Sauti ya Johannes)

“Kwa hiyo usaidizi wa mahitajiya kibinadamu Yemen siyo tu ni muhimu kwa misingi ya kibinadamu na kukidhi mahitaji  ya watu tunaowahudumia, bali pia ni njia ya kuendeleza utulivu wa nchi hiyo kwa muda mrefu.”

Amesema kwa wananchi wa Yemen, mabadiliko ya kisiasa ni lazima yaende na mabadiliko ya dhati kwenye maisha yao ya kila siku.