Vita dhidi ya Ebola yaingia kwenye awamu ya pili

23 Januari 2015

Shirika la Afya Duniani, WHO limesema mkakati wa Umoja wa Mataifa wa kutokomeza Ebola unaingia  awamu ya pili kutokana na kupungua kwa idadi ya visa vipya.

Mkurugenzi msaidizi wa WHO Bruce Aylward amesema hayo mjini Geneva Uswisi alipozungumza na waandishi wa habari  akieleza kwamba idadi ya visa vipya imeendelea kupungua kwa wiki nne mfululizo kwa mara ya kwanza tangu mwanzo wa mlipuko huo, mwelekeo huo ukileta matumaini ya kutokomeza kabisa ugonjwa wa Ebola.

Hata hivyo amesema juhudi zinahitajika ili kutokuwepo kabisa na visa vipya.

(Sauti ya Bruce)

Ili kutokomeza maambukizi, licha ya kupambana na matokeo ya ugonjwa tu, pia tunapaswa kuanza kupambana na mfululizo wa maambukizi. Hii inamaanisha kuelewa kikamilifu ni wapi maambukizi yanatokea, kubaini watu waliokuwa karibu na wagonjwa na kuwafuatilia ili kubaini maambukizi mapya kabla hawajaambukiza watu wengine”

Hadi leo, visa 21,797 vimeripotiwa, Sierra Leone ikiwa nchini iliyoathirika zaidi, wakati idadi ya visa vipya imepungua zaidi nchini Liberia.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter