Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNMEER yaipongeza Mali kwa kumaliza mlipuko wa Ebola

UNMEER yaipongeza Mali kwa kumaliza mlipuko wa Ebola

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu na Mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa kuhusu Dharura ya Ebola, UNMEER, Ismail Ould Cheikh Ahmed, ameipongeza Mali kwa kuumaliza mlipuko wa Ebola na kuitolea wito kuendelea kutahadhari wakati nchi jirani zikiendelea kuripoti visa vipya vya maambukizi.

Mnamo Januari 18 Umoja wa Mataifa ulitangaza rasmi kuwa mlipuko wa Ebola ulikuwa umekomeshwa Mali baada ya siku 42 bila kisa kipya cha maambukizi kuripotiwa. Kwa ujumla, watu 8 waliambukizwa kirusi cha Ebola nchini Mali, na sita kati yao wakafariki dunia, kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani, WHO.

Bwana Ismail Ould Cheikh Ahmed aliwasili Bamako mnamo Jumatano, akiubeba ujumbe wa Katibu Mkuu Ban Ki-moon, na pia kufanyia tathmini utaratibu wa kujiandaa kwa dharura ya uwezekano wa mlipuko wa visa vipya vya Ebola, kwani bado kuna idadi kubwa ya visa vipya vya maambukizi Guinea, Liberia na Sierra Leone, ingawa mwelekeo unabadilika sasa.

Wiki iliyopita, visa 145 vya Ebola vilithibitishwa , vikiwa ni miongoni mwa jumla ya visa 900 katika mwezi mmoja uliopita. Takriban jamii 50 zimeathiriwa katika nchi hizo tatu.