India yashirikiana na Umoja wa Mataifa kuimarisha utoaji wa tahadhari, miaka kumi baada ya Tsunami

26 Disemba 2014

Serikali ya India imetangaza leo kutoa mchango wa dola milioni moja kwa ajili ya mfuko wa ufadhili wa tume ya uchumi na kijamii kwenye ukanda wa Asia Pasifiki, ESCAP, kuhusu Tsunami, majanga na mabadiliko ya hali ya hewa.

Kwa mujibu wa ESCAP, mchango wa serikali ya India umeunga mkono juhudi za ESCAP ili kuimarisha mfumo wa kutoa tahadhari mapema kupitia ushirikiano wa kikanda. Pia umesaidia kuhakikisha kwamba tahadhari zinafikishwa haraka zaidi katika jamii zinazoishi kwenye mazingira magumu, ili kuokoa maisha na mali wakati wa majanga.

Katika taarifa iliyotolewa ijumaa, ESCAP imeeleza kuwa bado pwani za ukanda wa Asia-Pasifiki zinakabiliwa na hatari ya kupata maaafa kama tsunami au vimbunga.

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Mkuu wa ESCAP, Dkt. Shamshad Akhtar amekaribisha ushirikiano wa shirika lake na serikali ya India, akisema kwamba mfuko huo una rikodi nzuri katika kukuza ubunifu wenye suluhu katika ngazi ya kikanda.

Msaada huu umetolewa, ikiwa ni muongo mmoja baada ya kutokea kwa Tsunami ambapo zaidi ya watu 200,000 wamepoteza maisha.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud