Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chondechonde changieni CERF tuokoe maisha:Ban

Mtotot nchini Syria akipata chanjo ya surua katiak kambi ya wakimbizi ya Zaatari huko Jordan, moja ya misaada kutoka CERF. Picha/UNICEF

Chondechonde changieni CERF tuokoe maisha:Ban

Mfuko wa dharura wa majanga, CERF ni moja ya mambo muhimu yanayosaidia kuokoa maisha pindi majanga yanapoibuka, amesema Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon wakati akifungua kikao cha ngazi ya juu cha mwaka cha mfuko huo kilichofanyika sambamba na kusaka uchangiaji. Taarifa zaidi na Assumpta Massoi.

(Taarifa ya Assumpta)

Ban amesema CERF imekuwa kimbilio lakini kadri majanga yanavyoibuka duniani kote kila uchao kutokana na sababu mbali mbali ikiwemo za kiasili na za kibinadamu, mfuko huo unakuwa hautoshelezi.

Amesema mwaka huu pekee CERF imesaidia nchi 44 akitolea mfano utoaji chanjo kwa watoto, lishe kwa familia na hata kusafirisha wahudumu wa afya kwenda Afrika Magharibi baada ya mashirika ya ndege kusitisha safari kutokana na Ebola.

Pamoja na kutoa shukrani ameomba usaidizi zaidi kwani mfuko unaokoa maisha.

(Sauti ya Ban)

“Hatuwezi kutabiri majanga mapya mwaka 2015. Lakini tunachofahamu ni kwamba mamilioni ya watu wataendelea kuhitaji msaada. Mahitaji ni makubwa. Nawasihi kuchangia zaidi kwa moyo kwenye mfuko huu unaokoa maisha.”

Mwaka huu pekee, nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa wamechangia zaidi ya dola Milioni 460 kwa ajili ya operesheni za CERF, ikiwa ni zaidi ya kiwango kilichotarajiwa cha dola Milioni 450.