Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNAMID ipatiwe fursa ya kuchunguza tena Tabit:Ladsous

Afisa wa Jinsia akiongea na wanawake katika kambi ya Zam Zam yenye kuhifadhi watu waliokimbia makazi yao. Picha:UNAMID/Albert Gonzalez Farran

UNAMID ipatiwe fursa ya kuchunguza tena Tabit:Ladsous

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa hii leo limejadili hali ya usalama na janga la kibinadamu linalogubikwa na kuongezeka kwa uhalifu, ukwepaji wa sheria na raia kukimbia makazi yao katika jimbo la Darfur nchini Sudan. Assumpta Massoi amefuatilia mkutano huo

(TAARIFA YA ASSUMPTA)

Akihutubia kikao hicho Mkuu wa operesheni za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa, Hervé Ladsous amesema katika kutatua madhila ya wananchi jimboni Darfur ushirikiano kutoka serikali ya Sudan ni jambo lisilokwepeka akisisititiza kuwa raia wengi wanahitaji msaada wa mahitaji na ulinzi katika maeneo mengi.

Ameitaka serikali ya Sudan kutoa ushirikiano kwa maafisa wa ujumbe wa Umoja Mataifa na muungano wa Afrika jimboni Darfur, UNAMID kufika kijijini Tabit kuchunguza tuhuma za ubakaji wa wanawake.

(Sauti ya Ladsous)

"Kwa kweli uchunguzi zaidi unahitajika kwa sababu vikosi vya kijeshi na polisi walikuwepo kwa wengi katika kijiji hiki wakati UNAMID wanakwenda. Ni wazi tu kama UNAMID ikiweza kuchunguza kwa uhuru kabisa, ndiyo tutaweza kupata ukweli kuhusu madai hayo. Kwa hiyo naomba tena UNAMID ipatiwe fursa ya kufikia Tabit kwa haraka na uhuru ili kusikia raia wanasemaje na kubaini kilichotokea."

Kwa upande wake mwakilishi wa Sudan katika Umoja wa Mataifa Rahamtalla Mohamed Osman Alnor amesema kuwa taarifa za kuzuiwa kwa maafisa wa UNAMID kufika kijijini Tabit hazina ukweli na kwamba wanaruhusu maafisa hao kufika kijijini hapo.