Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban alaani shambulio la Jumanne huko Mandera, Kenya

Askari wa kikosi cha Afrika kinacholinda amani nchini Somalia, wakilinda daraja la mto Juba lililotwaliwa kutoka kwa Al shabaab. (Picha:AU/UN/IST/Mahamud Hassan)

Ban alaani shambulio la Jumanne huko Mandera, Kenya

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon amelaani vikali shambulio la kikatili dhidi ya wafanyakazi wa kiraia huko Mandera nchini Kenya.

Katika shambulio hilo la leo asubuhi watu 36 waliuawa ambapo Ban ametuma salamu za rambirambi kwa familia za wafiwa na serikali ya Kenya.

Taarifa ya msemaji wa Umoja wa Mataifa imemkariri Bwana Ban akisema anatarajia kuwa wahalifu wa tukio hilo wafikishwe mbele ya vyombo vya haki ili sheria ichukue mkondo wake.

Katibu Mkuu ameelezea mshikamano wa  Umoja wa Mataifa kwa Kenya kwenye harakati zake za kukabiliana na ugaidi na kutoa huduma za ulinzi kwa wananchi kwa mujibu wa sheria za kimataifa na misingi ya haki za binadamu.

Shambulio hili ni la pili ndani ya kipindi cha chini ya wiki mbili ambapo kikundi cha Al Shabaab kilidaiwa kuhusika na shambulio dhidi ya basi la raia kwenye eneo hilo hilo la Mandera lililo mpakani mwa Kenya na Somalia.