Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Serikali zisimamie sheria zinazolinda wanawake:UN-Women

@Picha ya UN Women

Serikali zisimamie sheria zinazolinda wanawake:UN-Women

Kuelekea siku ya kimataifa ya kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake, Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon pamoja na mkurugenzi Mtendaji wa shirika linalohusika na masuala ya wanawake kwenye Umoja huo, UN-Women, Phumzile Mlambo-Ngucka leo jioni watashiriki kwenye uwashaji taa za rangi ya chungwa kwenye jengo mashuhuri jijini New York, Empire State.

Taa hizo za rangi ya chungwa zitawaka kuanzia machweo sambamba na taa za jengo la makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, kuchagiza watu duniani kote kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake.

Akizungumza kiwango cha ukatili dhidi ya wanawake Bi. Mlambo-Ngucka anasema…

(Sauti ya Mlambo-Ngucka)

“Duniani kote mwanamke mmoja kati ya watatu amekabiliwa na kipigo au ukatili wa kingono katika maisha yake. Na miongoni mwa wanawake wote waliouawa mwaka 2012, nusu yao waliuawa na wanafamilia au wapenzi wao.”

Mkuu huyo wa UN-Women amesema hatua zaidi zinapaswa kuchukuliwa licha ya nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kuazimia kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake.

(Sauti ya Mlambo-Ngucka)

"Nchi nyingi tayari zina sheria sahihi lakini hazisimamiwi ipasavyo. Hili lazima libadilike. Serikali zina wajibu wa msingi wa kutekeleza sheria za sasa na mikataba na kuanzisha sheria mpya pale ambapo hakuna.”

Uwashaji wa taa za rangi ya chungwa na uvaaji wa nguo za rangi hiyo unang’oa nanga siku 16 za harakati dhidi ya ukatili wa kijinsia.