Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vyombo huru vya habari ni bora kwa ustawi wa jamii: UM

Waandishi wa habari wakitekeleza jukumu lao, hapa ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC. (Picha:UN/Sylvain Liechti)

Vyombo huru vya habari ni bora kwa ustawi wa jamii: UM

Katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa kumefanyika tukio la kutambua siku ya kutokomeza ukwepaji sheria kwa matukio ya udhalilishaji wa waandishi wa habari ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon amesema hakuna mwandishi wa habari popote pale duniani anayepaswa kuhatarisha maisha yake anaposaka habari.

Ban amesema hayo kwenye ujumbe aliotoa kwa njia ya video akisema kuwa vyombo huru vya habari ni msingi wa demokrasia na maendeleo hoja iliyotiliwa msisitizo na Kaimu Mkuu wake wa masuala ya mawasiliano, Maher Nasser.

(Sauti ya Nasser)

“Vyombo huru vya habari ni muhimu kwa jamii yenye ustawi. Vinasaidia kuweka uwajibikaji na utawala wa sheria. Vinawezesha kuwepo kwa utawala bora na huchangia mazingira muhimu kwa maendeleo.”

Umoja wa Mataifa unasema licha ya umuhimu huo, bado waandishi wa habari wanaendelea kuuawa akitolea mfano katika muongo mmoja uliopita waandishi wa habari 700 wameuawa wakitekeleza jukumu lao.