Ramos-Horta kuongoza jopo la kutathmini operesheni za amani

31 Oktoba 2014

Mabadiliko ya mwelekeo wa dunia hivi sasa hususan kwenye kusaka amani yanahitaji mbinu mpya na ndio maana Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon ametangaza kuunda jopo huru la ngazi ya juu kuhusika na operesheni za amani na ofisi za kisiasa.

Taarifa ya Msemaji wa Umoja wa Mataifa imesema jopo litaongozwa na Jose Ramos-Horta wa Timor-Letse na litakuwa na wajumbe wenye utalaamu kutoka nyanja mbali mbali.

Jukumu la jopo hilo ni kutathmini operesheni za sasa za amani za Umoja wa Mataifa na mahitaji yanayoweza kuibuka siku za usoni.

Mathalani litaangalia changamoto zinazokabili operesheni za ulinzi wa amani, kubadilika kwa aina za migogoro, ulinzi wa raia, haki za binadamu pamoja na uwezo wake.

Tathmini kubwa ya aina hiyo kwa mara ya mwisho ilifanyika mwaka 2000 na iliongozwa na Lahkdar Brahimi.

Mapendekezo ya jopo hilo yatawasilishwa wakati wa mjadala mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwakani 2015.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter