Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwaka 2014 umewezesha kutambuliwa kwa umuhimu wa kilimo cha kaya: FAO

Kilimo cha kaya ni msingi wa maendeleo siyo tu ya jamii bali taifa na dunia kwa ujumla.(Picha:FAO)

Mwaka 2014 umewezesha kutambuliwa kwa umuhimu wa kilimo cha kaya: FAO

Wakati mwaka huu wa 2014 uliotengwa kuwa mahsusi kwa kilimo cha kaya ukiwa unafikia ukingoni, Shirika la chakula na kilimo, FAO limesema hatua hiyo imewezesha kutambuliwa kwa jukumu adhimu la wakulima hao katika ustawi endelevu wa dunia.Mkurugenzi Mkuu wa FAO José Graziano da Silva amesema hayo mjini Rome, Italia katika siku ya kwanza ya mashauriano ya siku mbili ya kimataifa kuhusu mustakhbali wa kilimo cha kaya hata baada ya kumalizika mwaka huu.

Amesema moja ya mafanikio makubwa ni utashi wa kisiasa ulioonyeshwa mwaka huu katika kufahamu dhima ya wakulima wa kaya kwenye jukumu la siyo tu FAO bali pia kile dunia inataka na hatma endelevu ya wakazi wake.

Mathalani amesema kuangaziwa kwa kilimo cha kaya kwenye ajenda ya maendeleo baada ya mwaka 2015.

Hata hivyo amesisitiza umuhimu wa kuangalia siyo tu uzalishaji wa kilimo bali pia kutambua mashamba ya kaya kama maeneo ya kusambaza elimu na washirika wa lishe bora hususan shuleni.