Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwendesha mashtaka Mkuu ICC ahoji lugha za maazimio ya Baraza la Usalama

Fatou Bensouda, mwendesha mashtaka mkuu ICC. (Picha:Rick Bajornas)

Mwendesha mashtaka Mkuu ICC ahoji lugha za maazimio ya Baraza la Usalama

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa leo limekuwa na mjadala kuhusu mambo kadhaa ikiwemo ushirikiano kati ya chombo hicho na mahakama ya kimataifa ya uhalifu ICC. Joseph Msami amefuatilia mjadala huo

(TAARIFA YA MSAMI)

Akihutubia baraza hilo mwendesha mashtaka wa mahakama ya kimataifa ya uhalifu , Fatou Bensouda ameelitaka baraza hilo kutumia lugha kali na zenye mamlaka katika kufanikisha kufikishwa mahakamani kwa watuhumiwa ambao hati za kukamatwa zimeshatolewa na chombo hicho akitolea mfano wa Darfur na Libya  ambako licha ya hati kutolewa hatua stahiki hazijachukuliwa.

(SAUTI BENSOUDA)

“Kwa heshima kubwa natoa wito kwa baraza hili kuangalia uwezekano wa kutumia lugha yenye nguvu zaidi inapowasilisha maazimio yake sawa na lugha zilizotumika kwenye maazimio ya awali yakitaka ushirikiano kutoka nchi zote na mahakama ya kimataifa ya iliyokuwa Yugoslavia na ile ya Rwanda. Lugha iliyotumika kwenye maazimio kuhusu Darfur na Libya yanaacha utata mwingi iwapo kila nchi inawajibika kutoa ushirikiano.”

Mwendesha mashtaka huyo pia ametaka nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kutoa ushirikiano kwa ICC hususani pale hati ya kukamatwa inapotolewa kwa raia katika nchi hizo akionya kuwa mara kadhaa baadi ya nchi zimewahifadhi watuhumiwa wanaopaswa kufikishwa mahakamani.

Katika hatua nyingine kikao cha leo kimejadili juu vikwazo dhidi ya kundi la kigaidi la Alqaeda na makundi mengine katika kudumisha amani na utulivu.