Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maandalizi sahihi yatafanikisha vita dhidi ya Ebola: WHO

Madaktari kutoka Cuba walipowasili Sierra Leone kusaidia tiba dhidi ya Ebola. (Picha:WHO/S. Gborie)

Maandalizi sahihi yatafanikisha vita dhidi ya Ebola: WHO

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la afya duniani, WHO Dkt. Margaret Chan amesema kila nchi ina haki ya kujiandaa dhidi ya mlipuko wa Ebola kwani mazingira ya sasa duniani yanaweka nchi mbali mbali hatarini kupata ugonjwa huo.

Akizungumza huko Havana Cuba wakati wa mkutano wa nchi za Amerika Kusini na Karibea, ALBA uliolenga kutathmini harakati dhidi ya Ebola, Dkt. Chan amesema kila nchi  hususan zenye viwanja vya ndege vinavyohudumia safari za kimataifa ziko hatarini hivyo ni vyema kuchukua hatua.

Amesema maandalizi mema yanawezesha hatua sahihi za kujikinga na kuutokomeza ugonjwa huo akitolea mfano Nigeria ambayo imetangazwa kutokuwa na maambukizi mapya.

(Sauti ya Dkt. Chan)

Siku haipiti bila kusikia uvumi popote pale duniani wa kisa cha kuingia kwa mgonjwa wa Ebola kwenye uwanja wa ndege au kwenye chumba cha matibabu ya dharura eneo. Serikali ziko sahihi kuandaa vifaa vya kujikinga na kuonyesha vyumba vya kutenga wagonjwa. Hii inatoa hakikisho kwa wananchi na vyombo vya  habari kuwa nchi imejiandaa kudhibiti maambukizi zaidi iwapo mgonjwa anaingia nchini humo.”

Katika mkutano  huo, ujumbe wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ulisomwa na mjumbe wake maalum kuhusu Ebola Dkt, David Nabarro ambapo alishukuru Cuab na Venezuela kwa mchango wao wa hali na mali kwenye vita dhidi ya ugonjwa huo huko Liberia, Sierra Leone na Guinea.

Amekumbusha kuwa Ebola siyo hatari kwa ya eneo fulani pekee, bali una athari zake kiuchumi, kijamii na kiusalama na hivyo ni lazima kusaidia nchi zilizokumbwa kudhibiti ugonjwa huo.