Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ubia mpya wa FAO na National Geographic kuongeza uelewa kuhusu chakula

Chris Johns Mkuu wa maudhui wa National Geographic na Mkurugenzi wa FAO José Graziano.(Picha ya FAO)

Ubia mpya wa FAO na National Geographic kuongeza uelewa kuhusu chakula

Shirika la habari la National Geographic na Shirika la Chakula na Kilimo, FAO yanashirikiana katika kuongeza uelewa kuhusu masuala ya chakula na kilimo kupitia vipindi vitakavyotangazwa na National Geographic.

Msururu wa vipindi kuhusu mustakhbali wa chakula vitamulika suala la kulisha idadi kubwa ya watu inayoendelea kukua, na kuangazia masuala mseto yanayohusu chakula kote duniani.

Kaitlin Yarnall, ambaye ni Naibu Mkurugenzi wa Usanii katika jarida la National Geographic, anaeleza kuhusu ubia huo na jinsi National Geographic itakavyozitumia takwimu za FAO kutoa hadithi za masuala hayo.

Sauti ya Yarnall

Mwaka huu tumeangazia masuala muhimu kuhusu chakula na usalama wa chakula. Tulianza na kipindi kuhusu kulisha watu bilioni 9, tumemulika ufugaji wa majini na suala la haki za umiliki wa ardhi barani Afrika, na wiki hii tumetoa habari kuhusu ulaji nyama, tukiangazia Marekani, na mwezi ujao tuna kitu kuhusu, ‘furaha ya chakula’, yaani tunachokiita ‘uendelevu wa siri’: kitu kinachoangazia mchango wa kitamaduni wa chakula, na jinsi kinachotuleta pamoja.”

Bi Yarnall anaelezea zaidi kuhusu majukwaa tofauti ya matangazoyaona jinsi habari hizi zitasambazwa.

Sauti ya Yarnall

“Katika gazeti tunafanya makala inayotumia picha, habari za kina,  lakini nadhani kilicho  tofauti kuhusu mfululizo huu ni jinsi tunavyoiratibu kidijitali, kila kitu kinavyoonekana katika tovuti yetu ya natgeofood.net, pia tuna msururu wa mabloga wanaoonekana kwenye blogu yetu inayoitwa The Plate, yenye maoni ya aina yake kuhusu masuala ya chakula na kilimo, pia tuna maelezo kuhusu chakula kila siku, kisha katika habari kwenye tovuti yetu, tunamulika zaidi ufufuaji wa uzalishaji chakula na kilimo, mwaka mzima.”