Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban ahimiza juhudi zaidi Siku ya Kutokomeza Umaskini

Katibu Mkuu Ban Ki-moon.Picha ya UM/NICA

Ban ahimiza juhudi zaidi Siku ya Kutokomeza Umaskini

Leo Oktoba 17 ni Siku ya Kimataifa ya Kutokomeza Umaskini, na katika ujumbe wake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amesema kuwa siku hii ni ya kutafakari, kufanya uamuzi na kuchukua hatua pamoja dhidi ya umaskini uliokithiri, na kupanga kuwa na ulimwengu ambapo hakuna mtu anayeachwa nyuma.

Bwana Ban amesema kuwa ulimwengu umefikia lengo la maendeleo ya milenia la kupunguza idadi ya watu wanaoishi katika umaskini kwa nusu kabla ya terehe ya ukomo, na watu wapatao milioni 700 waliodolewa katika umaskini uliokithiri kati ya mwaka 1990 na 2010.

Licha ya mafanikio hayo makubwa, Katibu Mkuu amesema mtu mmoja kati ya kila watu watano, sawa na watu bilioni 1.22 katika nchi zinazoendelea, bado wanaishi kwa chini ya dola 1.25 kila siku, huku wengine bilioni 2.4 wakiishi kwa chini ya dola 2 kwa siku.

Ban amesema kuwa umaskini uliokita mizizi na ubaguzi, pamoja na mianya mikubwa kati ya utajiri na umaskini, vinaweza kudhoofisha ustawi wa jamii na kuchangia migogoro. Amesema, wakati huu inapoandaliwa ajenda ya maendeleo endelevu baada ya 2015, ni lazima kutokomeza umaskini uendelee kuangaziwa.