Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Rais wa Syria akiri kufanyika makosa wakati wa kukabiliana na waandamanaji

Rais wa Syria akiri kufanyika makosa wakati wa kukabiliana na waandamanaji

Rais wa Syria Bashar al-Assad kwa mara ya kwanza amekiri vikosi vyake vilifanya makosa wakati vikishughulikia maandamano ya raia wanaoupinga utawala wake.Rais Bashar ametoa kauli hiyo mbele ya ujumbe maalumu kutoka nchi za India, Brazil na Afrika Kusini unaotembelea nchi hiyo kwa ajili ya kupeleka ushawishi mpya wa maafikiano.

Mataifa hayo matatu ni wanachama wa umoja unaojulikana IBSA uliundwa kwa ajili ya kukaribisha mashirikiano zaidi miongoni mwao. Nchi hizo zimeendelea kutoa ushawishi mkubwa kwenye sera za kigeni.Akijadiliana na ujumbe huo, rais Bashar alitambulisha nia yake ya kukaribisha mageuzi ambayo ni moja ya mada inayopiganiwa na waandamanaji hao.

Katika taarifa yao kwa vyombo vya habari, ujumbe huo ulielezea masikitiko yake kuhusiana na namna vyombo vya dola vinavyoyadhibiti maandamano hayo na ikatoa mwito kusitishwa kwa vitendo vya mabavu.