Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkuu wa MONUSCO alaani mashambulizi Ochia

Martin Kobler@UN

Mkuu wa MONUSCO alaani mashambulizi Ochia

Mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuweka utulivu Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC, MONUSCO, Martin Kobler, amelaani vikali mauaji ya raia tisa na wanachama wanaotuhumiwa kuwa kundi la waasi la Uganda la ADF kilometre 30 kaskazini mwa Ochia, Beni, Mashariki mwa DRC.

Kobler amesema ameshtushwa na shambulizi hilo la kufedhehesha ambalo linaonyesha haja ya kuendelea na kuimarisha mapambano dhidi ya makundi ya waasi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, akisema vurugu lazima imalizike.

Mkuu huyo wa MONUSCO amesema watafanya kila wawezalo kusaidia serikali ya DRC kuangamiza kundi la ADF na makundi mengine ya waasi yanayowahangaisha wananchi wa DRC.

Shambulizi hilo lilitokea usiku wa tarehe Nane kuamkia tarehe Tisa wakati waasi walivamia Oicha, na kuwauwa watu 9 kutoka familia mbili wakiwemo watoto.

Shambulizi hilo lilisababisha kufurushwa kwa wakazi wengi wa eneo la Oicha, Beni, huku raia kati ya 3,000-5,000 wakiwasili Beni katika kipindi cha saa 24.