Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Posta imejikita kukabiliana na utandawazi: UPU

Posta imejikita kukabiliana na utandawazi: UPU

Ikiwa leo ni siku ya posta ulimwenguni, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Posta Duniani, Bashir A Hussein amesema huduma hiyo imejiandaa kuwa na dhima muhimu wakati huu wa zama za utandawazi na intaneti zinazolazimu ujumuishi wa raia kila kona.

Amesema wakati nusu ya wakazi wa dunia wanaishi vijijini, mtandao wa posta uko tayari kuwafikia akitolea mfano nchi za Afrika zilizo kusini mwa Jangwa la Sahara ambako ndiko kwenye ofisi nyingi za posta.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi, Bashir amesema pamoja na kufikia wananchi, UPU imejipanga kuimarisha huduma zake za kutuma na kupokea fedha.

Ametaja mradi wanaozindua tarehe 15 mwezi huu Geneva kwa ushirikiano na shirika la kimataifa la uhamiaji, IOM ili kuwezesha wahamiaji waBurundikutuma fedha nyumbani.

(Sauti ya Bashir)

"Wafanyakazi wahamiaji wamesambaa maeneo mengi duniani, na fedha wanazotuma ni kiasi kikubwa kuliko fedha zote za misaada zinatotolewa duniani kote. Na njia rahisi ya kutuma fedha hizo ni kupitia mtandao wa posta.”

Kwa mujibu wa benki ya dunia, ofisi za posta ndizo zenye huduma nafuu zaidi za kutuma na kupokea fedha ikifuatiwa na benki na kampuni nyinginezo.