Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatma ya kesi dhidi ya Uhuru Kenyatta kujulikana leo

ICC-CPI
Uhuru Muigai Kenyatta akiwa ICC, Hague tarehe 8 Oktoba 2014. Picha:

Hatma ya kesi dhidi ya Uhuru Kenyatta kujulikana leo

Kikao kuhusu hali ya  ushirikiano kati ya mahakama ya kimataifa ya uhalifu, ICC ya The Hague, Uholanzi na serikali ya Kenya kuhusu kesi dhidi ya Uhuru Kenyatta leo kinaingia siku ya pili.

Taarifa ya ICC imesema kikao hicho kilianza jana ambapo siku ya leo tarehe Nane mshtakiwa mwenyewe Kenyatta atakuwepo mahakamani.

ICC imesema kikao hicho kinajadili ushirikiano huo kwa kuzingatia hoja iliyotolewa na mwendesha mashtaka tarehe Tano mwezi uliopita.

Katika hoja hiyo, mwendesha mashtaka alisema kutokana na hali ilivyo hakuna ushahidi wa kutosheleza kumtia hatiani Kenyatta, kwa madai serikali inakwamisha utoaji ushahidi na hadhi ya urais ya mshtakiwa.

Jopo la majaji watatu katika mkutano huo wa leo litaongozwa na Jaji Kuniko Ozaki na wengien ni Jaji Robert Fremr na Jaji Geoffrey A. Henderson.

Kenyatta anashtakiwa kwa makosa matano ya uhalifu dhidi ya binadamu ikiwemo mauaji, ubakaji yanayodaiwa kutendwa wakati wa ghasia zilizoibuka baada ya uchaguzi mkuu waKenyamwaka 2007.