Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Njaa imepungua duniani, lakini bado watu milioni 805 hawana lishe ya kutosha

PIcha ya FAO/Paballo Thekiso

Njaa imepungua duniani, lakini bado watu milioni 805 hawana lishe ya kutosha

Takriban watu milioni 805 duniani bado wanaathirika na njaa mara kwa mara, kwa mujibu wa ripoti kuhusu ukosefu wa usalama wa chakula iliyotolewa leo na Shirika la Chakula na Kilimo FAO, Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo IFAD na Shirika la Chakula Duniani WFP. Taarifa zaidi na Priscilla Lecomte.

Matokeo ya ujumla ya ripoti hii yanaonyesha kwamba bado lengo namba moja la malengo ya maendeleo ya milenia ambalo ni kupunguza kwa nusu idadi ya watu walioathirika na njaa duniani linaweza kutimizwa ifikapo 2015, iwapo juhudi zinazohitajika zitaongezwa. Tayari idadi ya watu walioathirilka na njaa imepungua kwa milioni 200 tangu mwanzo wa miaka ya tisini.

Mkurugenzi Mkuu wa FAO Jose Graziano Da Silva, amesema miongoni mwa watu 805 wanaokumbwa na utapiamalo ni wakulima wadogo wanaotegemea kilimo cha familia kuishi na hawazalishi vyakula vya kuwatosheleza.

Hata hivyo amepongeza mifano ya mafanikio katika nchi 63 zilizofanikiwa kupunguza njaa.

“ Somo la msingi tunaloona ni umuhimu wa utashi wa kisiasa. Nchi maskini kama Malawi imejitahidi sana na uwezo wake mdogo wa fedha na nguvu kazi, kutokana na msimamo wa kisiasa wa serikali ya Malawi katika kutokomeza njaa na kuiweka kipaumbele.”