Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mladenov kuhudhuria mkutano kuhusu Amani na Usalama wa Iraq

Nikolay Mladenov@Picha/UNAMI

Mladenov kuhudhuria mkutano kuhusu Amani na Usalama wa Iraq

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Iraq, Nickolay  Mladenov leo amehudhuria  Mkutano wa Kimataifa kuhusu Amani na Usalama wa Iraq mjini Paris.

Katika hotuba yake kwa niaba ya Katibu Mkuu, Mladenov ameziomba nchi wanachama kushirikiana katika utekelezaji wa vikwazo vilivyopitishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa katika azimio la 2107 (2014), na kutoa wito kwa mataifa hayo kutokomeza mtiririko wa wapiganaji wa kigeni, fedha na msaada mwingine kwa vikundi vya wanamgambo nchini Iraq na Syria, na iwajibishe wahusika, waandaaji na wadhamini wa vitendo vya kutisha vya kigaidi, ambavyo kwa njia moja ni uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu.

Mladenov ameeleza kuwa makubaliano ya kimataifa ya kupambana na makundi ya Kiislam yenye msimamo mkali pia ni lazima yatawaliwe na sheria za kimataifa na kwa kuzingatia ulinzi wa raia.

Aidha, Mladenov amesema "ufumbuzi wa kijeshi pekee hautoshi," akiongezea, kuwa mchakato wa kisiasa na mpango wa kina wa kushirikisha jamii yote katika mpango wa maamuzi ya nchi utakuwa muhimu.