Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Upangaji wa matokeo michezoni ni uhalifu, uchunguzi kufanyika : UNODC

Upangaji wa matokeo michezoni ni uhalifu, uchunguzi kufanyika : UNODC

Kituo cha usalama wa michezo (ICSS) kwa kushirikiana na ofisi ya Umoja wa Mataifa ya makabiliano dhidi ya madawa na uhalifu (UNODC), leo kimetangaza kuanzishwa kwa makubaliano ya kukuza uchunguzi unaovuka mipaka na mashtaka dhidi ya upangaji matokeo na udanganyifu katika mashindano mbalimbali ya michezo .

Tangazo hilo limetolewa Doha, Qatar katika tukio maalum wakati wa mkutano wa 13 kuhusu kuzuia uhalifu ambapo makubaliano hayo mapya yanajikita katika uwezeshaji wa kimafunzo kwa tasisi nyeti za michezo, serikali na utekelezaji wa kisheria.

Katika tukio hilo mkurugenzi mkuu wa UNODC Yury Fedotov amesisitiza kuwa upangaji wa matokeo ni uhalifu kama mwingine na sio suala la kawaida kama ambavyo umekuwa ukichukuliwa katika jamii akitaka utizamwe kisheria na uchunguzi wa kina hasa kwa kuzingatia kuwa unahusishwa na uhalfu wa kupangwa, rushwa na utakasaji wa fedha chafu.

Washiriki katika utolewaji wa tangazo hilo muhimu katika sekta ya michezo wamesema suala hili lililoshamiri zaidi miaka 10 iliyopita linahitaji udharura wa mamlaka husika katika kulikomesha kisheria

Inakadiriwa kuwa kwa mwaka michezo 300 ya mpira wa miguu hupangwa matokeo yake barani Ulaya, dola zaaidi ya bilioni 400 zilitumika katika Kamari michezoni mwaka 2012 kote duniani huku asilimai 80 ya Kamari hizo zikifanyika kinyume na sheria.