Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Obama kuongoza mkutano wa Baraza la Usalama kuhusu magaidi mamluki

Samantha Power, Mwakilishi wa kudumu wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa akizungumza na waandishi wa habari. (Picha: Eskinder Debebe)

Obama kuongoza mkutano wa Baraza la Usalama kuhusu magaidi mamluki

Marekani ambayo inashikilia urais wa Baraza la Usalama kwa mwezi huu wa Septemba imetangaza mambo muhimu yatakayoangaziwa kwenye kipindi hicho ikiwemo mjadala wa ngazi ya juu kuhusu vitisho vya amani na usalama duniani vinavyosababishwa na vitendo vya kigaidi.

Ratiba imetangazwa na Mwakilishi wa kudumu wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Samantha Power.

(Sauti ya Balozi Samantha)

“Habari kubwa bila shaka ni ya tarehe 25 Septemba ambapo Rais Barack Obama ataitisha mkutano wa viongozi wa juu wa nchi wanachama wa Baraza la Usalama ili dunia iweze kutambua na kuchukua hatua dhidi ya ongezeko la wapiganaji magaidi wa kigeni. Hatua hii imechukuliwa kwa kuzingatia matukio ya miezi ya hivi karibuni ikiwemo kuenea kwa  ISIL huko Iraq na Syria pamoja na tukio la jana.  Tunashuhudia ongezeko la magaidi kutoka maeneo mbali mbali duniani wakiondoka makwao kwenda kupigana vita ugenini. Huko wanafanya vitendo vya kikatili na mara nyingi wanarejea makwao wakiwa na misimamo mikali wanayopata baada ya kushiriki vitendo hivyo.”

Amesema tayari Katibu Mkuu Ban Ki-Moon amekubali mwaliko wa kutoa taarifa kwenye mkutano huo na watasaka maridhiano ndani ya baraza hilo juu ya hatua kali za kuchukuliwa.

Balozi Power amesema katika mkutano huo watahamasisha ushirikiano wa kimataifa katika kudhibiti safari za magaidi mamluki huku wakichagiza mipango chanya mbadala kwa wapiganaji hao, ambapo watazungumzia nafasi ya Umoja wa Mataifa kwenye kutekeleza mipango hiyo.

Masuala mengine yatakayomulikwa ni mjadala wa wazi kuhusu watoto kwenye mizozo utakaofanyika tarehe Jumatatu ijayo.