Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama laongeza muda wa UNAMID

Mlinda amani wa UNAMID katika moja ya doria kuhakikisha usalama wa raia huko Khor Abeche. (Picha: Albert Gonzalez Farran, UNAMID)

Baraza la Usalama laongeza muda wa UNAMID

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo limekutana kujadili suala la amani na usalama barani Afrika ambapo pamoja na mambo mengine limeongeza muda wa ujumbe wa pamoja wa Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika huko Darfur, UNAMID kwa miezi kumi zaidi. Taarifa kamili na Assumpta Massoi.

(Taarifa ya Assumpta)

Azimio hilo nambari 2173 limepitishwa kwa kauli moja ambapo muda wa UNAMID sasa umeongezwa hadi tarehe 30 Juni mwaka 2015. Hata hivyo azimio limepunguza idadi ya wanajeshi kutoka 19,555 hadi 15,845 ilhali polisi wao watakuwa 1,583 kutoka 6,432.

Hata hivyo azimio limetambua mchakato unaoendelea wa mjadala wa kitaifa huku ikionyesha wasiwasi wake kuhusu kuzorota kwa hali ya kibinadamu huko Darfur na vitisho na mashambulizi dhidi ya watoa huduma za kibinadamu.

Mara baada ya azimio kupitishwa, mwakilishi wa kudumu wa Sudan kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Rahamtalla Mohamed Osman Elnor akazungumza.

(Sauti ya Balozi)

 Azimio ambalo mmelipitisha punde limeongeza muda wa UNAMID kwa miezi 10. Hata hivyo tumejizatiti kufikia malengo ya mchakato wa dhati wa mjadala wa kitaifa kabla ya kumalizika kwa muda huo wa miezi kumi. Hasa kwa kuzingatia mchango wa mchakato shirikishi wa kisiasa tumejizatiti kuachana na uhasama na kukubali kuwa yaliyopita sindwele tugange yajayo. Na pia ni wakati wa kuanza kutumia kifungu namba 24 cha azimio namba 1769.

 Baraza pia limepata taarifa kuhusu Libya ambapo Tarik Mitri Mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa Libya anayemaliza muda wake ameshukuru mchango wa Baraza hilo katika utekelezaji wa majukumu ya ujumbe huo ikiwemo kupambana na ugaidi.