Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNMISS yalaani kushikiliwa kwa waangalizi wa IGAD

Picha: UNMISS

UNMISS yalaani kushikiliwa kwa waangalizi wa IGAD

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa huko Sudan Kusini, UNMISS umelaani kitendo cha kushikiliwa kwa watu Tisa wakiwemo watendaji sita wa IGAD ambao walikuwa wanafuatilia utekelezaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano huko jimbo la Unity.

Taarifa ya UNMISS imesema watu hao walikamatwa siku ya Jumamosi huko Buoth, kilometa 35 kusini magharibi mwa mji mkuu wa jimbo la Unity, Bentiu na vikosi vilivyoasi kutoka SPLA.

Yaelezwa kuwa afisa mmoja wa SPLA ambaye alikuwa sehemu ya jopo hilo la uangalizi alifariki dunia akiwa kizuizini kutokana na ugonjwa. UNMISS iliwezesha kuwapata watendaji hao na kuwasafirisha kwa ndege hadi kituo chahe kilichoko Bentiu siku ya Jumapili.

Hata hivyo hadi sasa jitihada zinaendelea za kusaka ndege iliyotumika kuwasafrisha waangalizi hao hadi Bouth.

UNMISS katika taarifa yake imesisitiza kuunga mkono jitihada za IGAD za kuleta usuluhishi na kufuatilia mfumo wa utekelezaji wa usitishaji mapigano kama ilivyokubaliwa na pande zote kwenye mzozo wa Sudan Kusini tarehe 23 Januari mwaka huu.

Imetaka pande hizo kusaka suluhu ya amani na ya kudumu kwenye mzozo huo unaoendelea.