Tuvunje ukimya afya ya akili ya vijana: Ban, Ashe

12 Agosti 2014

Wakati leo ni siku ya kimataifa ya vijana ikiangazia afya ya akili ya kundi hilo, chapisho jipya la Umoja wa Mataifa linaonyesha kuwa asilimia 20 ya vijana duniani kote wanakumbwa na tatizo hilo kila mwaka.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon katika ujumbe wake wa siku hii amesema hali inakuwa mbaya zaidi kijana anapokuwa kwenye kipindi cha mpito cha kuwa mtu mzima kwani anakumbwa na unyanyapaa na kushindwa kusaka msaada anaohitaji.

Ban amesema maudhui ya mwaka huu ya afya ya akili ya vijana yamekuja wakati muafaka kwani yatasaidia vijana kuondoka kwenye kikwazo hicho cha kutengwa na ukimya na hatimaye kufikia ustawi wao.

Naye John Ashe ambaye ni Rais wa Baraza Kuu amesema siku hii ni fursa ya kuangazia mahitaji ya vijana wakati huu ambapo serikali zinajadili malengo 17 ya maendeleo endelevu baada ya mwaka 2015.

Amesema pamoja na hiyo, ni muhimu zaidi kuangazia afya ya akili ya vijana katika harakati zao kwani wengi wao hukumbwa na ubaguzi na hivyo kushindwa kufikia malengo yao ya ustawi.

Kuadhimisha siku hii hapa makao makuu ya Umoja wa Mataifa kutakuwepo na tukio maalum likihusisha mijadala ya wazi na tumbuizo kutoka kwa wasanii vijana.

Tukio hilo litahudhuriwa na wawakilishi wa ngazi ya juu wa vijana kutoka nchi mbalimbali pamoja na Ban na Ashe.