Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Heko SLA/Minni Minawi kwa kuchukua hatua kuepusha watoto jeshini:UNAMID

Watoto hawa wacheza katika kituo cha jamii kilichojengwa na UNAMID katika kambi ya wakimbizi wa ndani , Khor Abeche, kusini Darfur (Picha/UM/Albert González Farran/NICA)

Heko SLA/Minni Minawi kwa kuchukua hatua kuepusha watoto jeshini:UNAMID

Ujumbe wa pamoja wa Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika huko Darfur, UNAMID, umekaribisha hatua mpya ziliyochukuliwa na kikundi kilichojihami cha Sudan Liberation Army/Minni Minawi, SLA/Minni Minawi cha kupiga marufuku uandikishaji watoto kwenye vikosi vyake.

Naibu Mkuu wa UNAMID Abidoun Bashua amesema hatua hiyo inatokana na agizo la mkuu wa kikundi hicho Minni Minawi aliyoitoa mwezi Disemba mwaka jana baada ya kushiriki mafunzo huko Addis Ababa, Ethiopia kuhusu Amani na usalama Darfur.

Kundi hilo lilishatangaza amri yake ya kuzingatia masharti na maadili ya kimataifa yanayolinda haki za watoto na Sheria ya Mtoto ya Sudan ya mwaka 2010.

Hata hivyo tarehe Sita mwezi huu limeweka bayana kamati ya utekelezaji ambayo siyo tu itaelimisha askari wake kuhusu agizo hilo bali pia litashirikiana na taasisi mbali mbali kurejesha na kutangamanisha askari watoto kwenye jamii.

Bashua amesema huu ni mwelekeo mzuri unaochangia katika juhudi za pamoja za Sudan na UNAMID ili kutokomeza utumikishwaji wa watoto jeshini huko Darfur akiongeza kwamba kulinda haki za watoto ni msingi wa amani endelevu.

Tangu mwaka 2009, zaidi ya watoto 1,200 wamesharudishiwa makwao kupitia miradi wa kupokonya silaha, kuvunja vikosi na kurejeshwa katika jamii, DDR, unaotekelezwa kwa ushirikiano baina ya serikali ya Sudan, UNICEF na UNAMID.