Benki ya dunia yatoa dola Bilioni Tano kukuza umeme Afrika, Tanzania na Kenya zimo

Watoto darasani.Picha@world bank

Benki ya dunia yatoa dola Bilioni Tano kukuza umeme Afrika, Tanzania na Kenya zimo

Benki ya dunia itatoa dola Bilioni Tano kwa ajili ya kuimarisha uzalishaji umeme kwenye nchi sita za Afrika, tangazo lililotolewa na Rais wa benki hiyo Jim Yong Kim wakati wa mkutano wa viongozi wa Afrika na Marekani mjini Washington. Taarifa zaidi na John Ronoh.

(Taarifa ya John Ronoh )

Nchi hizo ni Kenya, Tanzania, Ethiopia, Ghana, Liberia na Ghana ambazo Dkt. Kim amesema zitapatiwa usaidizi wa kiufundi na kifedha kutekeleza miradi ya kuzalisha umeme.

Amesema usaidizi huo wa dharura unahitajika barani humo ambako watu Milioni 600 hawana umeme licha ya kwamba Afrika ina baadhi ya vyanzo vikubwa duniani vya kuzalisha umeme kwa njia ya maji, jotoardhi, upepo, jua na gesi asilia.

Kupitia fedha hizo, amesema Benki ya dunia na Marekani sasa zinaandaa majukumu na mwelekeo utakaowezesha kufikia robo la lengo la Afrika la kuzalisha megawati 10,000 za umeme huko Afrika Kusini mwa jangwa la Sahara.

Naye Makamu wa Rais wa Benki ya dunia anayeshughulikia Afrika, Makhtar Diop amesema Afrika kama ilivyo Ulaya na maeneo mengine duniani ina haki sawa na kutumia vyanzo vyake vizuri vya nishati ili kuinua maisha na ustawi wa watu watu.