Hakuna mahali salama kwa watoto wa Gaza- Zerrougui

30 Julai 2014

Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Watoto na mizozo ya silaha, Leila Zerrougui, amesema kuwa baada ya wiki tatu za vita katika Ukanda wa Gaza, hakuna mahali salama kwa watoto wa Gaza.

Bi Zerrougui amesema hayo leo baada ya shule nyingine ya Umoja wa Mataifa inayohifadhi zaidi ya wakimbizi 3,300 kupigwa na makombora yaliyovurumishwa na wanajeshi wa Israel hata baada ya jeshi hilo kufahamishwa na Umoja wa Mataifa kuwa shule hiyo inatumika kuhifadhi wakimbizi.

Kufuatia shambulizi hilo, raia pamoja na watoto waliuawa na wengine kujeruhiwa, jambo ambalo Bi Zerrougui amelaani vikali na kutaja kuwa ukiukwaji wa sheria za kimataifa.

Zaidi ya raia 250,000 wamelazimika kuhama makaazi yao. Bi Zerrougui amesema shule na vifaa vingine vinavyotumika na jamii na watoto vinapaswa kuheshimiwa na kulindwa kwa vyovyote vile.

Amesema, wakati mapigano yakiendela kuzidi, watoto wamekutwa katikati na ni vigumu kuwalinda ipasavyo. Amesema wakati asilimia 40 ya eneo zima la Ukanda wa Gaza likiathiriwa na mzozo na kutangazwa kuwa eneo la hatari, raia hawana tena pa kukimbilia kutafuta usalama. Takwimu zinaonyesha kuwa tokea tarehe 7 Julai hadi sasa, zaidi ya robo ya idadi ya watu wote waliouawa ni watoto, idadi yao ikiwa imezidi 25

Amesihi pande zote kusitisha mapigano na kuheshimu sheria za kimataifa, haki za kibinadamu, ulinzi wa shule na hospitali na pia kulinda wafanyakazi wa huduma za kibinadamu.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud