Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zaidi ya dola Bilioni 2.4 zaahidiwa ili kuikwamua Syria

Zaidi ya dola Bilioni 2.4 zaahidiwa ili kuikwamua Syria

Mkutano wa pili wa kimataifa wa usaidizi wa kibinadamu kwa Syria umemalizika hukoKuwait ambapo zaidi ya dola Bilioni 2.4 zimechangishwa ikiwa ni ahadi. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa akizungumza na waandishi wa habari baada ya mkutano huo amesema kiasi kamili cha fedha kitatangazwa baadaye lakini ahadi hiyo ni ishara dhahiri kuwa wahanga wa mzozo wa Syria hawajasahaulika na ndio maana mashirika na hata nchi zimejitoa kwa hali na mali kusaidia wananchi hao.

Bwana Ban amesema Umoja wa Mataifa utahakikisha fedha hizo zinatumika ipasavyo ili kuwapatia mamilioni ya wahanga wa mzozo wa Syria huduma muhimu kama vile maji, chakula, malazi, matibabu ya dharura na huduma nyingine muhimu.

Katibu Mkuu amesema jumuiya ya kimataifa imejitoa kwa moyo kwenye masuala ya kiutu na sasa kilichobakia ni kuleta pamoja pande zinazozozana Syria ili mkutano wa wiki ijayo huko Uswisi uweze kuzaa matunda.