Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNAIDS na wadau wazindua mkakati wa kuimarisha vipimo vya HIV

Picha@UNAIDS

UNAIDS na wadau wazindua mkakati wa kuimarisha vipimo vya HIV

Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na masuala ya ukimwi UNAIDS, kwa ushirikiano na Shirika la Afya Duniani, WHO na lile la kuhudumia watoto UNICEF, na wadau wengine, limezindua mkakati wa vipimo ambao unahimiza kuboresha uwezo wa maabara kuhakikisha kwamba watu wanaoishi na virusi vya HIV wanaweza kupata huduma stahiki kwa matibabu ya HIV.

Mkurugenzi Mtendaji wa UNADIS, Michel Sidibé amesema kwamba takriban watu milioni 19 kati ya watu milioni 35 wanoishi na virusi vya HIV hawajui hali yao, huku akiongeza kwamba ni muhimu kurahisisha utaratibu wa kupimwa HIV ili kuweza kutafuta matibabu.

Kulingana na UNAIDS, lengo la mkakati huo ni kuhakikisha kwamba takriban asilimia 90 ya watu wanaoishi na virusi vya HIV wanajua hali yao. Aidha, unalenga kuhakisha kwamba watu wanaopokea matibabu ya HIV wanapata huduma ya karibu waliko kuchunguza idadi ya kirusi katika miili yao ili kuhakikisha matibabu sahihi.

Kwa sasa nchi chache tu ambazo zinaubeba mzigo mkubwa wa HIV ndizo zinatoa huduma ya upimaji wa idadi ya virusi kwa watu wanaopokea matibabu ya HIV.