Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF yatiwa moyo na ahadi za serikali kupunguza vifo vya uzazi

Mama na mtoto wake aliyedhaifu wakitoka katika kituo cha afya cha UNICEF katika mkoa wa Maradi. Picha@ UNICEF/Olivier Asselin(UN News Centre)

UNICEF yatiwa moyo na ahadi za serikali kupunguza vifo vya uzazi

Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na watoto UNICEF limeelezea matumaini yake ya kukabiliana na vifo vya kina mama wajawazito na watoto walio chini ya umri wa miaka mitano kutokana na msukumo uliotolewa na serikali katika kongamano moja la kimataifa lililomalizika huko Afrika Kusini.

UNICEF imesema kuwa ahadi zilizotolewa na serikali ambazo zimesema kuwa zitaongeza nguvu kukabiliana na changamoto inayojitokeza kwenye sekta ya uzazi ni matumaini tosha kwamba kampeni ya kukabiliana na vifo vitokanavyo na uzazi sasa inaweza kufanikiwa.

Takwimu za UNICEF zinaonyesha kwamba kiasi cha watoto milioni 2.9 hupoteza maisha katika miezi yao ya kwanza ya uhai huku milioni 1 hawafikishi hata siku moja tangu wanapozaliwa na kuna wasiwasi kwamba idadi hiyo huenda ikaongezeka kama kutakosekana hatua za haraka.

Kongamano hilo la kimataifa lililozinduliwa na mke wa rais wa zamani wa Afrika Kusini Graca  Machel lina lengo la kuongeza msukumo wa kukabiliana na tatizo linaloandama sekta ya uzazi ili kupunguza idadi hiyo ya vifo.