Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Utipwatipwa wasababisha vifo vya watu Milioni 2.8 kila mwaka duniani:Mtaalamu

Anand Grover mtaalamu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki ya chakula. Picha@UN maktaba

Utipwatipwa wasababisha vifo vya watu Milioni 2.8 kila mwaka duniani:Mtaalamu

Mtaalamu maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki ya afya Anand Grover amesema ongezeko la watu tipwatipwa duniani limetokana kwa kiasi kikubwa na mfumo wa sasa wa ulaji wa vyakula vya hovyo.

Grover amesema vyakula hivyo vyenye kiwango kikubwa cha sukari, mafuta yenye lehemu pamoja na wanga yanasababisha ongezeko la vifo vitokanavyo na magonjwa yanayohusiana na mlo.

Katika ripoti yake ya mwisho kwa Baraza la haki za binadamu huko Geneva, Uswisi, Grover ameonya kuwa takwimu za sasa zinachukiza akitolea mfano kuwa watu zaidi ya Bilioni Mbili duniani ni matipwatipwa ilhali wengine Milioni 2.8 hufariki dunia kila mwaka kutokana na uzito kupita kiasi.

Lawama kuwa ni milo ya hovyo yenye kiwango kikubwa cha sukari, chumvi na mafuta yenye lehemu ambayo sasa kwa bahati mbaya imechukua nafasi ya vyakula vyenye afya kwenye milo yetu, amesema Grover.

Amesema sera za utandawazi na uimarishaji wa masoko unaofanywa na kampuni za kimataifa na maduka makubwa pamoja na vitegauchumi vya kigeni vimebadili mfumo wa ulaji kwenye jamii na kulata milo isiyo na afya.

Ili kubadili mwelekeo amependekeza pamoja na mambo mengine serikali kutunga sera za kugusa sekta zote zinazolenga kuendeleza upatikanaji wa vyakula vyenye afya na kuwapatia wananchi taarifa kuhusu mlo sahihi.