Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban azungumza na Rais mteule wa Ukraine, ataka uchaguzi uimarishe amani:Feltman

Mkuu wa masuala ya siasa ndani ya UM, Jeffrey Feltman (Picha@Maktaba UM)

Ban azungumza na Rais mteule wa Ukraine, ataka uchaguzi uimarishe amani:Feltman

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo limekuwa na kikao cha mashauriano kuhusu hali ilivyo nchini Ukraine hasa baada ya uchaguzi wa Rais tarehe 25 mwezi huu na kuelezwa kuwa bado kuna ghasia katika baadhi ya maeneo.

Kikao hicho kilifanyika kufuatia ombi la Uingereza ambapo Mkuu wa masuala ya siasa kwenye Umoja wa Mataifa Jeffrey Feltman alisema wengi walijitokeza kupiga kura lakini baadhi ya maeneo hususan huko Mashariki mwa Ukraine baadhi ya wapiga kura waliokuwa na haki ya kufanya hivyo walinyimwa haki hiyo kutokana na sababu mbali mbali.

Ametaja sababu hizo kuwa ni pamoja na majengo kushikiliwa, baadhi ya vituo vya kupiga kura kuzuiliwa, vifaa vya uchaguzi kuharibiwa au vitisho na ghasia, jambo ambalo linatia shaka…

(Sauti ya Feltman)

 

“Umoja wa Mataifa una masikitiko sana na vitendo vya hao ambao wamejaribu kupeleka mrama uchaguzi kwa kuzuia raia kuamua uongozi wa nchi yao.”

Amesema leo Katibu Mkuu wa  Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon amezungumza kwa njia ya simu na Rais Mteule wa Ukraine, Petro Poroshenko na kumpongeza kwa kuungwa mkono kwa kiasi hivyo na hivyo…

 (Sauti ya Feltman)

 “Tunamtaraji achukue hatua haraka na kuondoa nchi kwenye mzozo wa kisiasa, kiuchumi na kijamii na kuipeleka kwenye usalama, ustawi zaidi, matumaini na utawala wa dhati wa kidemokrasia.”

 

Feltman pamoja na kueleza kuwa  jamii ya kimataifa itumie matokeo ya uchaguzi ya Ukraine kama fursa ya kuungana na kusaidia amani na ustawi wa nchi hiyo, amezungumzia madai ya  kwamba helikopta za Umoja wa Mataifa zimeonekana Ukraine.

(Sauti ya Feltman)

 “Napenda kutambua kuwa mamlaka za Ukraine zimethibitisha kwa Umoja wa Mataifa kuwa hakuna helikopta yenye alama za Umoja wa Mataifa ambazo zinatumika kwenye operesheni ndani ya Ukraine.”