Shambulio Kabul lasababisha vifo vya watu 14; Ban, Baraza la Usalama walaani vikali

Shambulio Kabul lasababisha vifo vya watu 14; Ban, Baraza la Usalama walaani vikali

Nchini Afghanistan, watu 14 wameuawa na wengine wengi wamejeruhiwa kufuatia shambulio la Ijumaa kwenye mgahawa mmoja katikati mwa mji mkuu Kabul. Miongoni mwa waliouawa ni raia wa nchi hiyo na wa kigeni wakiwemo wafanyakazi wanne wa Umoja wa Mataifa.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon ameshutumu vikali shambulio hilo na kusema kuwa matukio ya aina hiyo ya kulenga raia hayakubaliki na ni kinyume na sheria za kimataifa. Ametuma risala za rambirambi kwa wafiwa na kutakia ahueni ya haraka majeruhi.

Wakati huo huo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa nalo limetoa taarifa ya kushutumu tukio hilo ambapo wajumbe wamesema halikubaliki. Wamesisitiza mshikamano wao na shughuli za Umoja wa mataifa nchini Afghanistan pamoja na mashirika mengine yenye ubia na umoja huo katika harakati za kuimarisha usalama.

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan, UNAMA imesema kikundi cha Taliban kimedai kuhusika na shambulio hilo ambapo wajumbe wa baraza la usalama wameelezea hofu yao juu ya vitisho vinavyotoka kwa kikundi hicho. Wamesema ugaidi haukubaliki kwa misingi yoyote ile na wamezungumzia umuhimu wa kuwafikisha wahusika wa shambulio hilo mbele ya sheria.

Wamerejelea msimamo wao kuwa hakuna tukio lolote la ugaidi linaloweza kubadili mwelekeo wa amani, demokrasia na utulivu unaoongozwa na wananchi wenyewe wa Afghanistan kwa ushirikiano wa serikali na jamii ya kimataifa.